Dk Slaa kupanda ‘kizimbani’ leo SOMA HAPA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad
Slaa, leo anatarajiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Hai
kutoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili kijana aliyejifanya
Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alisema jana kuwa Dk Slaa amethibitisha kuitikia wito huo wa Mahakama.
Katika ushahidi uliotolewa mahakamani,
Dk Slaa akiwa Mtendaji Mkuu wa Chadema, ndiye anayedaiwa kushughulikia
suala la mshtakiwa kutaka kuwatapeli viongozi wa Chadema.
Tayari Jaji Samatta na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema wamekwishatoa ushahidi wao katika kesi hiyo
inayoendeshwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Katika ushahidi wake, Jaji Samatta
alikana kumfahamu mshtakiwa Abeid Adam Abeid (22) na kwamba namba ya
simu iliyotumiwa kujitambulisha kwa Dk Slaa na Lema kuwa ni Jaji Samatta
siyo yake.
Kwa upande wake, Lema alidai mshtakiwa
huyo alimtumia meseji mbalimbali akijitambulisha kwake kuwa ni Jaji
Samatta na kwamba angemsaidia katika rufaa yake ya kuvuliwa ubunge ya
mwaka 2012.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili
wa Takukuru, Susan Kimaro ulidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya
Aprili na Mei 2012. Mtuhumiwa alikana mashtaka hayo na leo upande wa
mashtaka unatarajiwa kufunga ushahidi wao baada ya Dk Slaa na shahidi
mwingine ambaye hajatajwa, kutoa ushahidi wao.
0 comments: