SIASA: Aliyetemwa ukuu wa wilaya ya Igunga ageukia ubunge
Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu.
Siku
moja baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa
mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu amesema sasa anageukia ubunge
katika Jimbo la Singida Magharibi.
Kingu
alisema siku nyingi alikuwa na shauku ya kugombea ubunge katika jimbo
hilo, kwamba kuondolewa katika wadhifa huo kutampa nafasi ya kujipanga
na kuhakikisha anashinda jimbo hilo linaloongozwa na Mohamed Hamisi
Missanga (CCM).
“Unajua
kwa muda sasa akili yangu ilijikita zaidi katika ubunge ili niweze
kuwasaidia wananchi kwa ukaribu zaidi. Wananchi wa Jimbo la Singida
Magharibi wamekaa muda mrefu bila kupata mtu wa kutatua matatizo
yanayowakabili,” alisema.
Alifafanua
kuwa Februari 28, mwaka huu atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika
jimbo hilo, ataitumia siku hiyo kutangaza rasmi nia yake ya kugombea
ubunge.
“Nitakachokifanya
sasa ni kuwa karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha matatizo
yanayowakabili ninayajua kiundani ili niweze kuyatatua kwa urahisi,”
alisema.
Aliongeza,
“Namshukuru Rais Kikwete kwani aliniamini na kazi aliyonipa niliifanya
kwa uaminifu na uzalendo wa hali ya juu, kufanikiwa kuleta mabadiliko
katika sekta ya kilimo, afya, mifugo, uvuvi na maendeleo kwa vijana,”
alisema Kingu (pichani).
“Rais ameamua nipumzike na ninamshukuru kwa uzalendo wake mkubwa naamini bado ana imani kubwa na mimi.”
Akitoa ushauri wa wakuu wapya wa wilaya alisema, “Wanatakiwa kuhakikisha wanamsaidia kazi Rais Kikwete na kutekeleza ilani.”
Wakati
Kingu akieleza hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,
Zelothe Stephen ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma.
Alisema:
“Sina maneno mengi kwa sasa nitasema kauli tatu; Asante kwa pongezi
yako, namshukuru Mwenyezi Mungu, namshukuru sana Rais Kikwete kwa
kuniteuwa kushika wadhifa huu.”
Kwa
upande wake Martha Umbulla aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto,
alipotafutwa siku nzima ya jana alisema kuwa yupo katika kikao na
kuahidi kuzungumzia uteuzi huo baada ya kumalizika kwa kikao, jambo
ambalo hakulitekeleza.
Wilaya
ya Kiteto ni moja kati ya wilaya zilizokithiri migogoro ya ardhi kati
ya wakulima na wafugaji, iliyosababisha watu zaidi ya 10 kuuawa na
wengine kujeruhiwa.
Akizungumzia
uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Bara, John Mnyika alisema
unadhihirisha kuwa nchi ina mifumo legelege ya kupima wanaopendekezwa
kuteuliwa kabla ya uteuzi.
“Uteuzi
huu unapaswa kuibua mjadala wa haja ya kufuta wadhifa wa ukuu wa
wilaya. Watanzania wanatakiwa kuikataa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu
imependekeza vyeo vya wakuu wa wilaya ambavyo vipo kwa ajili ya kufanya
hujuma na kuiba kura katika chaguzi,” alisema.
Hata
hivyo, mkurugenzi wa masomo ya shahada ya kwanza kutoka Chuo cha
Usimamaizi wa Fedha (IFM), Dk Shaban Ngole alisema kuwa mabadiliko
yaliyofanywa kwa wakuu wa wilaya yanalenga kukiimarisha chama tawala
baada ya tathmini ya matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Ndiyo
maana unaweza ukaona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanazua maswali
katika jamii, mfano, uteuzi wa Paul Makonda hauna kitu kingine zaidi ya
kuongeza ushawishi wa chama katika Wilaya ya Kinondoni. Chama kimeona
kuwa anaweza kuhimili mikikimikiki ya hapa mjini,” alisema Dk Ngole.
Alifafanua
kuwa Makonda anaeleweka kuwa ni kada wa CCM ambaye hajifichi kutokana
na utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya chama hicho, hivyo kuteuliwa
kwake hakuwezi kuwa na maana nyingine.
Licha
ya kukiimarisha chama, Dk Ngole alisema kuwa Serikali ina dhamira ya
kuongeza ufanisi katika utendaji wake. Hilo limeisukuma kufanya
mabadiliko ya msingi ili kujiongezea nafasi ya ushawishi miongoni mwa
wananchi.
0 comments: