Kingunge: Waliojitokeza kuwania urais CCM hawana sifa
Harakati
za kuwania urais ndani ya CCM zimeingia katika hatua mpya baada ya
mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru kuibuka na kudai kuwa wote
waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha
kutaka kuingia Ikulu.
Kauli
ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja kabla ya Kamati Kuu ya CCM
kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda ikitajwa kuwa suala la
maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa hao ambao wanaongezeka
kila kukicha.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Kingunge alisema: “Kuna suala la kukosa uadilifu,
kuna suala la matumizi ya pesa na nikwambie ukweli, hao wanaotangaza
urais wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi
wanajua.”
Kwa
miezi kadhaa sasa, baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakitajwa kufanya
harakati kichinichini na wengine kushiriki shughuli za wazi
zinazoashiria kuwa wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu. Hadi sasa makada
wanne tayari wameweka wazi nia yao hiyo.
Hivi
karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli zinazowashutumu makada wengine
wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya fedha katika kushawishi uungwaji
mkono.
Hata
hivyo, kauli za wanasiasa hao zimedaiwa kuwa ni fitina za kisiasa kwa
kuwa wagombea wote wanatoa fedha, bali wanazidiana viwango tu.
Mbali
na Makamba na Membe, wanaCCM wengine waliotangaza au kutajwa kuwania
urais ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine
ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kauli
ya Kingunge aliyoitoa kupitia Televisheni ya ITV, imekuja wakati
wanasiasa sita miongoni mwa hao wanaotajwa wakikaribia kumaliza miezi 12
ya uangalizi kutokana na onyo kali dhidi yao lililotolewa na Kamati Kuu
ya CCM Februari 18, mwaka jana baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya
“kuanza kampeni mapema na kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya
chama na ya jamii.”
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Lowassa, Sumaye, Njeleja, Makamba, Wasira na Membe.
Akisisitiza
hoja yake hiyo bila kutaja majina, Kingunge alisema makada hao wamekuwa
wakitumia fedha nyingi kujitangaza na kutengeneza ushawishi wa
kukubalika kwa wananchi jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi.
Kingunge alisema mwanasiasa yeyote anayehitaji uongozi hapaswi kutumia fedha kushawishi wananchi wamchague.
0 comments: