Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Asema ni yule mwenye makengeza, Asisitiza kuwa ni mtafuta fedha
Mbunge
wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, ‘amefunguka’ kuhusu kashfa
inayomkabili ya kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwenye fedha
zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), akisema hastahili kuitwa mwizi, bali anapaswa
kuitwa ‘nyoka wa makengeza’.
Amesema
anapaswa kuitwa ‘nyoka wa makengeza’ kwa kuwa yeye ni mjanja wa
kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wa jimbo lake, ambao wanapaswa
kupuuza madai ya wizi yanayoelekezwa kwake, badala yake wamwamini zaidi.
Chenge,
ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, alisema hayo
wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Mahaha kata ya Bunamala, Wilaya Bariadi mkoani Simiyu juzi.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa kimya, lakini ameshangazwa na kitendo cha kuandamwa kuhusiana na kashfa ya akaunti hiyo.
“Wanasema
Chenge na Escrow…Pale nimeenda kutafuta kwa ajili ya wananchi wa jimbo
langu wala sikwenda kubomoa duka. Bali tunatumia akili kutafuta pesa kwa
ajili yenu,” alisema Chenge.
Chenge
alitoa kauli hiyo wiki chache baada ya kusimama bungeni na kusema
amelazimika kufanya hivyo baada ya kumvumilia Mbunge wa Kawe (Chadema),
Halima Mdee, aliyetaka wabunge wachunguzwe kuhusiana na kashfa ya
akaunti hiyo na wa kwanza kuchunguzwa awe Chenge.
Alisema
kama Mdee ana ushahidi wa tuhuma anazozielekeza kwake, aupeleke bungeni
kama kanuni za Bunge zinavyotaka au tuhuma hizo akaziseme nje ya ukumbi
wa Bunge.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, mimi ningelipenda Bunge hili liendelee kuwa na heshima
yake. Pili, naomba sana hayo wanayoyasema wawe na ujasiri wa kwenda
kuyasema nje ya ukumbi huu wa Bunge, wasijifichie katika immunity
(kinga) ya Bunge,” alisema Chenge.
Alisema
anayo mengi ya kusema, lakini kwa sababu alisimama kuhusu utaratibu,
kumtaja yeye kwa jina moja kwa moja, anaomba aweke ushahidi mezani.
Mdee
alitoa pendekezo hilo wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya PAC
na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), bungeni, Januari 30, mwaka
huu.
Alisema Chenge amekuwapo katika kashfa mbalimbali za ufisadi, kuanzia ile inayohusu mikataba mibovu.
Kashfa
nyingine za ufisadi ambazo alisema Chenge ameshiriki ni pamoja na
inayohusu kampuni ya kufua umeme ya Independent Tanzania Limited (IPTL).
Nyingine alisema ni ya hivi karibuni ambayo alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 zilizochotwa kifisadi katika akaunti hiyo.
“Tuanze kuchunguzana wabunge, tuanze na Chenge,” alisema Mdee.
Kauli hiyo ya Mdee ndiyo iliyoonyesha kumkera Chenge na kulazimika kusimama bungeni siku hiyo na kutoa kauli hizo.
Kwa
mujibu wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), fedha
zinazodaiwa kuchotwa kutoka akaunti hiyo, ni zaidi ya Sh. bilioni 300
wakati kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, ni Sh. bilioni 202.9.
Chenge
alitajwa kupata mgawo huo kutoka katika fedha hizo na taarifa maalum ya
PAC iliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjombe, bungeni Novemba 26, mwaka
huu.
Taarifa
hiyo ya PAC, ilimtaja Chenge kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka
kwenye fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo.
Wengine
waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kupata mgawo kutoka katika fedha
hizo, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6), Mbunge wa Sengerema
(CCM), William Ngeleja (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa
Sumbawanga Mjini (CCM), Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).
Pia
wamo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh.
milioni 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), Jaji Profesa John
Ruhangisa (Sh. milioni 404.25), Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. milioni
40.4) pamoja na Mkurugenzi mstaafu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).
Wengine
ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole
Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8); Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la
Bukoba, Dk. Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.9); Askofu Msaidizi wa
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa (Sh. milioni
40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).
Kutokana
na taarifa hiyo ya PAC iliyohusu ukaguzi maalum wa malipo yaliyofanyika
katika akaunti hiyo, Novemba 29, mwaka jana, Bunge lilipitisha maazimio
nane dhidi ya wote waliohusika na kashfa hiyo.
Ukaguzi
huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Taarifa
hiyo ya PAC, ilieleza kuwa mmiliki wa kampuni ya Pan African Power
Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi, mmiliki wa kampuni ya VIP
Engineering & Marketing (VIP), James Rugemalira, walihusika kwa
namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya
fedha katika akaunti hiyo kwenda kwa kampuni hizo.
Wengine
waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa hiyo ni Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, Eliakim Maswi na
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo,
aliyejiuzulu.
Prof.
Muhongo alitajwa na taarifa hiyo ya PAC kuwa alikuwa dalali kati ya
Rugemalira na Sethi kufanikisha uchotwaji wa fedha hizo kutoka katika
akaunti hiyo.
Wengine
waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa hiyo, ni
pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick
Werema na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco).
Hivyo,
Bunge likaazimia kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya
ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria kwa mujibu wa
sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika na
vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti hiyo na
wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ya PAC, vitendo vilivyofanywa na watu hao
vinaashiria makosa mbalimbali ya jinai, kama vile uzembe, wizi,
ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka,
rushwa na kupokea mali ya wizi.
Tayari
Prof. Muhongo na Jaji Werema walikwishajiuzulu nafasi zao serikalini,
huku Maswi, ambaye amesimamishwa kazi akiendelea kuchunguzwa.
Pia
tayari Prof. Tibaijuka ameshatimuliwa kazi na Rais Kikwete kwa kupokea
fedha hizo kupitia akaunti yake binafsi iliyoko benki ya Mkombozi,
kinyume cha maadili.
Pia
kutokana na kashfa hiyo, Chenge, ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Bajeti, alijiuzulu nafasi hiyo kutekeleza moja ya maazimio
ya Bunge yaliyotaka yeye na waliokuwa wenyeviti wenzake wa kamati za
Bunge; Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa
(Nishati na Madini), wavuliwe nyadhifa hizo. Wote walijiuzulu nyadhifa
hizo.
Mbali
na kujiuzulu, Februari 2, mwaka huu, Baraza la Maadili lilitangaza
kuwaita kwa nia ya kuwahoji wabunge hao, akiwamo Prof. Tibaijuka,
Ngeleja, Mwambalaswa na Chenge, kutokana na tuhuma za kashfa ya akaunti
hiyo zinazowakabili.
Wabunge hao watafika mbele ya Baraza hilo, kuanzia Februari 23, mwaka huu.
Ofisa
Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo,
alisema mahojiano hayo yatafanyika kwa wiki tatu na yataongozwa na Jaji
mstaafu, Hamisi Msumi na wajumbe wengine wawili, Hilda Gondwe na Celina
Wambura.
MIRADI MAENDELEO JIMBONI
Akizungumzia
suala la wananchi na miradi ya maendeleo jimboni mwake, Chenge alisema
mtaji wa maendeleo ni kila mwananchi kujituma katika kuchangia miradi
mbalimbali na kushirikiana na viongozi na serikali kwa manufaa yao.
“Ndugu
zangu, ni bora miradi tunayoileta vijijini mwenu mkaitunza ili
tuendelee kuwatumikia kwa muda mrefu…na tufanye kazi ya kuilinda miradi
hiyo na kuisimamia miradi yote iliyo ndani ya kata hii,” alisema Chenge.
Mbunge
huyo alitembelea maabara ya Shule ya Sekondari Sapiwi kuangalia
maendeleo ya ujenzi wake baada ya Mfuko wa Jimbo kutoa mabati 300 kwa
ajili ya kuezekea maabara.
Shilingi milioni 36 zimetumika kugharimia ujenzi huo, huku wananchi wakichangia Sh. milioni 10 na Sh. milioni 74 zikihitajika.
Awali,
Ofisa Mtendaji wa kata ya Sapiwi, Telen Nhandi, alisema zipo changamoto
zinazoikabili kata hiyo ikiwamo upotoshaji wa watu katika michango ya
kuchangia maabara, ukame na kusababisha mazao mengi kuanza kuathirika.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia katika miradi ya maendeleo.
0 comments: