index

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatimua wanachama wake 42 wakiwemo wagombea walioshindwa kupita kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi karibuni.


Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, kutimuliwa kwa wanachama wake hao ni hatua ya chama hicho kujisafisha kutokana na kile kinachodaiwa kwamba baadhi ya wagombea hao wanatuhumiwa kufanya hujuma wakati wa mchakato wa uchaguzi serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.


Akitangaza uamuzi huo mjini humo, Katibu wa Chadema Jimbo la Korogwe Mjini, Ezekiel Mbwilo alisema wahusika waliotimuliwa uanachama wanatuhumiwa kwa kukubali vitisho na wengine kurubuniwa kwa fedha za wapinzani wao, hatua iliyowalazimu kwenda kuondoa majina yao katika hatua za mwisho kuelekea kwenye kinyang’anyiro hicho.


“Tuligundua kuwa baadhi ya wahusiska walijihusisha na hujuma mbalimbali dhidi ya chama chetu, ikiwamo kukubali kupewa fedha na wapinzani wao ili wajiondoe. Tangu awali, tulishakubalina kwamba ikibainika watu waliofanya hujuma tutawatimua kundini na hapa ndipo tunahitimisha lile tulilokubaliana,” alisema.


Mbwilo alitaja maeneo wanayotoka wanachama hao waliotimuliwa na idadi yao kwenye mabano ni Kwamsisiwatu (6), Mahenge (10), Kitifu (25) pamoja na mmoja kutoka Manundukati ambaye alidai kwamba mhusika huyo aliamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi ukiwa katika hatua za mwisho baada ya kurubuniwa na wapinzani wa chama hicho.


Akizungumzia vitisho alivyodai vilitolewa baadhi ya wanachama wa vyama vingine dhidi ya wagombea wa Chadema, Mbwilo alisema tayari amewasilisha taarifa hizo kwenye vyombo vya usalama na katika jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi.

0 comments: