Watatu wafukiwa na kifusi wakichimba madini wilayani Kahama mkoani Shinyanga





Wachimbaji watatu wa madini ya dhahabu ya Kalole kata ya Lunguya wilayani Kahama mkoani Shinyanga  wamefariki dunia baada ya kufukiwa na udongo wakiwa kwenye shimo la dhahabu wakitafuta dhahabu.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Januari 7,2015 saa 12 asubuhi katika machimbo madogo ya dhahabu ya Kalole kata ya Lunguya,tarafa ya Msalala wilayani Kahama.

Aliwataja waliofariki kwa kufukiwa kwenye shimo  hilo la dhahabu kuwa ni  Kulwa Magele(20) mkazi wa Shishani wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Ihalu Maheme(23) mkazi wa Idisa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu na Lameck Frank(22) mkazi wa Nzega mkoani Tabora.

Kamanda Kamugisha alisema vijana hao ambao ni wachimbaji wadogo wa madini waligundulika wakiwa wamekufa ndani ya shimo la kuchimbia dhahabu na inaelezwa kuwa waliingia kwenye shimo hilo ambalo halitumiki kwa nia ya kuchimba dhahabu ndpo likabomoka na kuwafukia na kusababisha  vifo vyao papo hapo.
Wakati huo huo mwanamke aitwaye Sayi Shitunguru(50) mkazi wa  kijiji cha Buruma kata ya Isaka wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa kitu kizito kichwani na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake.

Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Januari 7,2015 saa 1 asubuhi ambapo mwanamke huyo akiwa nyumbani kwake alivamiwa na mtu/watu wasiojulikana kasha kumpiga na kitu kizito kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo.

Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana  na jeshi la polisi linaendelea kufanyan uchunguzi ili kubaini chanzo chake.

Hata hiyvyo alisema tayari wanamshikilia mtu mmoja aitwaye  John Jota(33) mkazi wa Kazungu wilayani Kahama kwa mahojiano zaidi huku akiwataka wananchi kushirikiana na polisi ili kusaidia kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.

0 comments: