MMILIKI WA IPTL ATEMA CHECHE...JAJI MKUU AGOMA KUZUNGUMZIA...STANBIC NAYO YAKANA KUHUSIKA HUKU NAIBU WAZIRI WA NISHATI MASELE AJIGAMBA NA KUSEMA NI SAWA NA KUMPIGA CHURA TEKE NA KUMWONGEZEA MWENDO KWAHIYO SIOGOPI!

Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh.

Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh amesema anafikiria mara mbilimbili iwapo aendelee kuwekeza nchini au la, baada ya kuwapo kwa tuhuma kwamba alihusika na uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nimeongelewa sana kiasi kwamba naona kama hakuna hata amani ya kuwekeza Tanzania, nitajifikiria mara mbili mbili. Wananchi wanaelewa vingine kabisa kuhusu suala hili kwa sababu ya upotoshwaji,” alisema Singh alipozungumza na gazeti hili jana.
Singh ambaye alituhumiwa kujipatia asilimia 70 ya hisa katika Kampuni ya IPTL isivyo halali, alisema hafikirii kuwekeza zaidi nchini kwa sababu yamekuwapo maneno mengi na shutuma zisizo na ukweli zilizoelekezwa kwake kuhusu sakata hilo.
Kauli ya bosi huyo wa IPTL imekuja wakati Taifa likisubiri utekelezaji wa maazimio ya Bunge na akiwa mmojawapo wa watu wanaotakiwa kuchunguzwa na vyombo vya dola ili akibainika kufanya makosa, afikishwe mahakamani.
Jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza haraka maazimio manane yaliyotolewa na Bunge dhidi ya ufisadi wa sakata la escrow.
“Rais hatakiwi kukaa kimya, atoe tamko la haraka ili kuwaondoa viongozi hao. Hata Waziri Mkuu anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu ni chanzo cha udhaifu huo,” alisema Profesa Lipumba alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF (JUKECUF).
Jana, Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema alisema: “Kwangu ni kama hukumu imetangulia mashtaka kwa sababu sikuwahi kuitwa kuhojiwa mahali popote, ila ninauheshimu uamuzi wa Bunge.”
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema hayuko tayari kuzungumzia masuala ya kashfa ya Akaunti ya Escrow pamoja na mwingiliano wa mihimili miwili, Bunge na Mahakama kwa kuwa siyo wakati wake.
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa Benki ya Stanbic Tanzania nao ulitoa taarifa ya kukana kuhusika katika utakatishaji fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya Bunge kupitisha azimio la kuitaka mamlaka husika za kifedha kuichunguza.
Malamiko ya Singh
Singh alisema kampuni yake imekuwa ikiuza umeme kwa bei nafuu; senti nane kuliko kampuni nyingine, lakini bado anaonekana kuwa na makosa.
“Kuuza umeme kwa senti nane kwa megawati ni bei nafuu sana lakini mbona naonekana kama nina makosa? Ndiyo maana ninasema nitafikiria mara mbili kuwauzia umeme,” alisema.
Alisema kampuni nyingine za kufua umeme zinauza umeme mara mbili ya bei kuliko yake, lakini bado anaonekana si mwekezaji mzuri huku mazuri yote aliyoyafanya nchini yakisahauliwa.
Alisema anashangazwa na kauli za wabunge na baadhi ya wanasiasa kuwa anatakiwa kukamatwa kwa kukwepa kodi na kujipatia fedha isivyo halali na kusema haoni kosa alilolifanya mpaka sasa.
“Wanikamate kwa lipi? Hata kutaifisha mali zangu au mitambo hawawezi kabisa hiyo ni kazi ya Mahakama,” alisema.
Alisema wanaomtuhumu kuwa kaiba fedha za umma hawana hoja na kwamba kama ingekuwa kweli, waliotakiwa kulalamika ni mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemalira na raia wa Malaysia, aliyemtaja kwa jina moja la Barbin... “Wenyewe wahusika hawajasema kama wameibiwa lakini leo naambiwa na Bunge nimeiba na wanataka kutaifisha mali zangu inashangaza sana.”
Alisema ameshangazwa na jinsi Bunge lilivyomhukumu bila kupewa nafasi ya kujitetea... “Wao wanajadili bungeni, Mahakama haijatoa hukumu lakini wanamhukumu mtu ambaye hayupo hapo, hawajasikia utetezi wake. Inashangaza sana, kwa nini Mahakama isifanyie kazi suala hili na kutoa hukumu?”
Kuhusu utata wa uraia wake, Singh alisema hakuna ukweli wowote kuwa yeye ni Mkenya au wa Afrika Kusini na kusisitiza kuwa ni Mtanzania, mzaliwa wa Iringa. “Mimi ni Mtanzania, unafikiri mimi Mhindi?” alihoji Singh.
Kauli ya Ngeleja
Kwa upande wake, Ngeleja naye alilalamikia kutohojiwa na kusema: “Siwezi kufahamu kwa nini sikuitwa kuhojiwa maana hata maaskofu nimesikia kwenye vyombo vya habari kwamba nao wanalalamika hawakuhojiwa, pengine inawezekana muda ulikuwa mfupi, hilo sifahamu.”
Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla ya kung’olewa katika nafasi hiyo alisema katika mazingira ya sasa hawezi kuzungumzia fedha zinazodaiwa kuingizwa katika akaunti yake, hadi pale wenye mamlaka zitakapotekeleza maazimio ya Bunge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko alisema anasubiri uchunguzi ufanyike ili kubaini ukweli juu ya kuhusishwa na mgawo wa Sh40.4 milioni zilizochotwa kutoka akaunti hiyo.
“Unataka nizungumze nini sasa? Taarifa zimesomwa na kutangazwa, tusubiri huo uchunguzi unaotakiwa kufanyika,” alisema.
Jaji Mkuu agoma
Akizungumza baada ya mkutano wa viongozi wa Mahakama na vyombo vya habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Jaji Mkuu Chande alisema: “Mambo hayo yameshajadiliwa na hapa tulipo si mahala pake.”
Aliombwa kutoa kauli yake kuhusu baadhi ya majaji kuhusishwa na kashfa ya hiyo na kile kilichoelezwa kuwa kuingiliana kwa mihimili ya Bunge na Mahakama katika kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Mahakama aliyekuwapo eneo hilo, alisema suala majaji wanaotuhumiwa linanasubiri kuundwa kwa tume ya kijaji kama ilivyoelekezwa na Bunge.
Majaji hao waliotajwa ni Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa ambao wanadaiwa kuhamishiwa fedha kutoka kwa akaunti ya mmojawapo wa watuhumiwa iliyopo Benki ya Mkombozi. Hadi sasa majaji hao hawajatoa maelezo yoyote kuhusu suala hilo.
Stanbic yakana
Benki ya Stanbic jana ilitoa taarifa kwa umma ikisema haihusiki na sakata hilo na kwamba imekuwa ikifuata sheria na kanuni za kifedha katika utendaji wake.
“Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba Benki ya Stanbic siku zote inafuata masharti yote na pamoja na sheria za maadili zilizowekwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki ilishatoa taarifa ikikanusha kuhusika kutakatisha fedha chafu.
“Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhuma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu,” ilisema taarifa hiyo.
Msemaji wa BoT, Lwaga Mwambane alisema tuhuma dhidi ya benki hizo zinafanyiwa kazi na Kitengo cha Intelijensia ya Fedha (FIU) kilichopo chini ya Wizara ya Fedha.
Masele ajigamba
Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele amejigamba kuwa tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake kuhusu sakata hilo ni kama kumpiga chura teke na kumwongezea mwendo.
Akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Serikali za Mitaa mjini Shinyanga juzi, Masele alisema aliokolewa kutoka kwenye mto uliojaa mamba na kusema wabaya wake walijua tayari wamemwangamiza na kwamba kupona kwake kumempa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko katika jimbo lake la Msalala.
chanzo:gazeti la mwananchi

0 comments: