WARIOBA NA ZITTO WAJADILI ESCROW KWA MASAA MAWILI




Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (kushoto), akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe. Masaki Dar es Salaam jana.

Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba juzi alifanya mazungumzo ya saa mbili ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kuhusu masuala ya uongozi na uwajibikaji baada ya mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kumtembelea nyumbani kwake, Masaki, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Zitto pia alimweleza Waziri Mkuu huyo mstaafu maazimio ya Bunge kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika ujumbe wake mfupi alioutuma katika mtandao wa Facebook, Zitto alisema: “Nimekuwa na mkutano wa zaidi ya masaa mawili (saa mbili) na Mzee Warioba kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yetu kama uongozi na uwajibikaji. Pia nimemweleza kwa ufupi kuhusu maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.”
Kukutana kwa viongozi hao kumekuja ikiwa zimepita siku mbili tangu Jaji Warioba kuzungumza na gazeti hili kuhusu sakata la escrow na maazimio manane ya Bunge.
Zitto alimtembelea Jaji Warioba siku habari hiyo ilipochapishwa, kitendo ambacho kimetafsiriwa kama ni mbunge huyo kutolea ufafanuzi maoni ya Jaji Warioba ambaye pia amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hasa kuhusu maeneo yaliyoachwa katika ripoti hiyo licha ya kuwa yanaonekana kuhusika katika kashfa hiyo.
Bunge lilihitimisha mjadala wa kashfa hiyo, kwa kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
Bunge hilo pia liliazimia kuwajibishwa kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco pamoja na wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge; Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na William Ngeleja (Bajeti).
Katika maoni yake juu ya kashfa hiyo, Jaji Warioba alisema Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo zinahusika.
Alisema katika Ripoti ya CAG na PAC, wametaja ukiukwaji wa malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gain) na ushuru wa stempu (stamp duty) na kuwa wanaohusika katika hilo ni Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na upande mwingine ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ambao uko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Alisema hata kampuni iliyotajwa kuwa imesajiliwa Brela inaonyesha katika ripoti kuwa wahusika walioisajili hawakuweka majina yao, bali saini tu.
Alifafanua kuwa uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya Nishati na Madini lakini hasara iliyotajwa kuonekana inazihusu zaidi Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na kusisitiza kuwa uamuzi wa Bunge ulitawaliwa na mchezo wa siasa, kwamba baadhi walindwe na wengine waachwe.
Jaji Warioba alisema kasoro nyingine ni kitendo cha watu wanaodaiwa kupewa fedha na James Rugemalira kutajwa majina yao sambamba na akaunti ya aliyewapa, lakini wale waliodaiwa kuchota fedha hizo katika magunia hawakutajwa.
Pia, alisema haamini kama fedha za escrow ni za Serikali na kuhoji kama zingekuwa za umma zingewekwa katika akaunti hiyo kwa misingi ipi?
Katika maazimo yake Kamati ya PAC ilieleza kuwa uchunguzi kuhusu sakata hilo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ulieleza kuwa fedha za umma zinaweza kuwamo katika akaunti hiyo.
SOURCE: MWANANCHI

0 comments: