RAIA WA PAKISTAN AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 60 JELA KWA KOSA LA KUSAFIRISHA TWIGA WANNE HAI KWENDA QATAR.

Moshi/Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, jana imemhukumu raia wa Pakistan Ahmed Kamran kifungo cha miaka 60 jela baada ya kumtia hatiani kwa makosa manne ikiwamo kusafirisha twiga wanne hai kwenda Qatar.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Simon Kobelo, ambaye pia aliamuru kutaifishwa kwa mali zote za mtuhumiwa huyo zilizopo katika ardhi ya Tanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana baada ya kutolewa hukumu hiyo, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema kilichofanyika ni kutaka kuonyesha haki imetendeka, huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, James Lembeli akisema kuwa kumsaka mtuhumiwa huyo ni sawa na mchezo wa kuigiza.
Hata hivyo, tayari Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) juzi limewataka Watanzania kusaidia katika kumsaka Kamrani, huku likitangaza kuanzisha operesheni iliyoipa jina la Infra Terra ikilenga kuwanasa watuhumiwa uharamia zaidi ya 139 katika nchi 36 duniani.
Mchungaji Msigwa alisema kuwa kilichofanyika ni kiini macho kwa kutaka kuonyesha kuwa haki imetendeka. Alisema haiwezekani Ahmed apatikane na kosa pekee yake wakati mchakato wa kusafirisha wanyama unaonyesha watu wengi wakiwamo viongozi walishiriki kutekeleza biashara hiyo.
“Hata kama wangemfunga miaka 200 haisaidii kitu, hapo mahakama imefanya kazi yake lakini Serikali inafanya kiini macho,” alisema Msigwa.
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, alisema kitendo cha mahakama kuthibitisha kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa na vibali halali kinaonyesha kuwa kuna baadhi ya watu walishiriki kumtorosha ili wasitiwe nguvuni.
“Isingewezekana ndege iingie nchini bila wakubwa kujua ilikuja kufanya nini?” alihoji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema kumsaka mtuhumiwa Kamran Ahmed anaona huo ni mchezo kwa sababu mtuhumiwa huyo raia wa Pakistan alishatoroka awali kisha akapatikana, lakini katika hali ya kushangaza akapewa tena dhamana.
Lembeli alisema hatua ya kuruhusu dhamana ya pili kwa mtuhumiwa huyo inatia shaka kuwa kuna jambo lisilo la kawaida lililomwezesha kutoroka kwake.
“Hivi kwa nini walimpa dhamana wakati alishatoroka mara ya kwanza na huyu mwandishi Temba aliyemdhamini sijui alianzia wapi, najua hamfahamu lakini amejiingiza kwenye matatizo ya kujitakia,” alisema Lembeli.
Kuhusu ndege inayodaiwa kutumika kusafirisha wanyama hao, ambapo mahakama imethibitisha kuwa ilikuwa na vibali vyote halali vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia, Lembeli alisema Wizara ya Mambo ya Nje ieleze kwa kina jambo hilo lilitokeaje.
“Mimi katika hilo sitaki kuzungumza sana, ila nafikiri kuna haja ya kujiridhisha kuwa kibali hicho cha kidiplomasia ni cha aina gani, kilitolewaje, kisha majibu tutakayopata ndipo tutajua nini kilitokea,” alisema Lembeli.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na naibu wake, Mahmoud Mgimwa, simu zao ziliita bila kupokelewa.
Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa bila mtuhumiwa wa kwanza (Kamran) kuwapo mahakamani baada ya kutoroka tangu Februari mwaka huu wakati kesi yake ikiwa katika hatua za mwanzo za usikilizwaji.
Katika hukumu hiyo, hakimu Kobelo aliwaona washtakiwa wengine wanne, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu kuwa hawana kesi ya kujibu na kuwaachia huru.
Hakimu Kobelo alisema hakuna ubishi kuwa raia huyo wa Pakistan (Kamran), ndiye aliyekuwa wakala katika biashara hiyo na ambaye ndiye aliyewasafirisha wanyama hao kwa kutumia ndege kubwa ya Jeshi la Qatar. Kobelo alisema ndege hiyo ilikuwa na vibali vyote halali vya kuingia nchini kwa safari ya kidiplomasia kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA).
Hakimu Kobelo alisisitiza kuwa ndege iliyobeba wanyama hao ilikuwa na hadhi ya kidiplomasia na ilifuata taratibu zote na kuruhusiwa na mamlaka za nchi ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje.Uchambuzi wa ushahidi huo unaonyesha raia huyo wa Pakistan, aliruhusiwa na mamlaka za Tanzania kukamata wanyama kwa kutumia leseni za kampuni mbili zinazomilikiwa na Hawa.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuwa na kibali cha kusafirisha wanyama hao kwenda nje ya nchi na kwa kuwa alitoroka, mahakama haikuweza kupata uthibitisho wake kama alikuwa na kibali.
Kutokana na uchambuzi huo, mahakama imemtia hatiani raia huyo wa Pakistani kwa makosa manne ambapo kila kosa amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

0 comments: