Polisi Mwanza watumia risasi za moto kulinda mkutano wa Machinga


Maelfu ya wafanyabiashara ndogondogo mjini Mwanza, wamefanya uchaguzi wa viongozi wa umoja wa machinga jijini Mwanza huku ulinzi mkali wa askari Polisi wenye silaha za moto na mabomu ya machozi ukiwa umeimarishwa kwenye uwanja wa CCM kirumba ili kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani.
Mkutano huo wa uchaguzi ambao ulifunguliwa na katibu tawala wa wilaya ya nyamagana Marcella Mayala, ulitawaliwa na zomeazomea, shangwe na vigelegele wakati wagombea wa nafasi mbalimbali walipokuwa wakijinadi, huku baadhi ya machinga wakihoji zilipo fedha zao zaidi ya shilingi milioni 10 zilizotolewa na rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Dk. Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuwasaidia machinga kukopeshana ili kuinua biashara zao.
 
Baadhi ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti waliokuwa wakishangiliwa wakati wakijieleza kuomba kura ni pamoja na Said Tembo, Richard Mushi na Kabaila Liberatus. 
 
Kila mgombea aliwahakikishia machinga kupata maeneo mazuri ya kufanyia biashara pamoja na kumaliza kilio cha muda mrefu cha kukamatiwa mali zao na askari mgambo wa jiji.
 
Uchaguzi wa umoja wa machinga jijini mwanza unafanyika kufuatia machinga kukosa viongozi kwa muda mrefu na hadi paparazi wetu anaondoka katika uwanja huo wa CCM kirumba, zoezi la upigaji kura lilikuwa limekamilika katika nafasi zote zinazowaniwa.
 
Na habari zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa Said Tembo amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa umoja wa machinga jijini mwanza.

0 comments: