10 wajeruhiwa ajali ya Noah wakitoka Maulid

Mmoja wa majeruhi, Mwanahawa Ramadhani, akiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza kupatiwa matibabu baada ya kuvunjika mkono kutokana na ajali ya gari wakitokea Bagamoyo mkoani Pwani kusherehekea Maulid. 
Watu 10 wamejeruhiwa baada ya gari dogo aina ya Noah kupinduka katika kijiji cha Kitumbi Wilaya ya  Handeni mkoani Tanga.

Ajali hiyoilitokea juzi gari hilo likiwa limebeba abiria wanawake watupu waliokuwa wakitoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kusherehekea sikukuu ya Maulid kuelekea kijiji cha Kwakibuyu kata ya Songa wilayani Muheza.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,  Frasser Kashai, abiria waliopata ajali hiyo walikuwa wakitoka katika Msikiti wa Songa kwa Kibuyu wilayani Muheza.

"Walikodi magari mawili yote aina ya Noah moja liliwabeba wanaume na lingine wanawake kwa ajili ya kuwapeleka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kusherehekea Maulid," alifafanua Kamanda Kashai.

Alifafanua kuwa baada ya Maulid kumalizika, waligeuza siku iliyofuata kurejea Muheza.

Alisema kuwa gari iliyokuwa imewabeba wanawake, ilitangulia mbele na kufuatiwa ya wanaume.

Hata hivyo, Kamanda Kashai alisema walipofika maeneo ya kijiji cha Kitumbi, gari lililokuwa limewabeba wanawake, lilipinduka na kusababisha majeruhi hao.

Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva kutaka kulipita gari lingine ambapo lilitokea gari lingine mbele yake na alipojaribu kulikwepa, likapinduka

Baadhi ya majeruhi walivunjika mikono katika ajali hiyo.

Sheikh Mkuu wa kata ya Songa, Twaha Saidi, alimueleza Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, aliyekwenda kuwajulia hali majeruhi hao katika Hospitali Teule Muheza kuwa majeruhi wote walioumia ni waumini wa dini ya Kiisilamu na walikuwa wanatoka katika Maulid wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Na katika hatua nyingine, majeruhi sita wa ajali ya ajali ya basi dogo aina ya Hiace wakati wakitokea kijiji cha Misozwe kuelekea mjini Muheza mjini, wamelazwa Hospitali Teule Muheza, wametoa kilio kwa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu,  wakidai  kwamba tangu wapate ajali hiyo zaidi ya wiki moja sasa, hawajapatiwa huduma yoyote ya matibabu.

Kutokana na kilio cha majeruhi hao, Mgalu amewaagiza viongozi wa hospitali hiyo kuwashughulikia haraka majeruhi hao ikiwamo na kuwapiga picha za X-ray.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya, ameahidi kwamba atafika hospitali hapo kila siku kusikiliza kero za majeruhi hao.

0 comments: