Yanga yamtema Kaseja rasmi, yamdai 400m


Kipa wa Yanga Juma Kaseja.

YANGA imetangaza rasmi kuachana na kipa Juma Kaseja lakini Championi Ijumaa linafahamu ukweli kuwa klabu hiyo imepanga kumfungulia mashitaka ya kumtaka alipe shilingi milioni 400, kutokana na kuvunja mkataba.
Akitangaza kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro alisema kuwa Kaseja ndiye aliyevunja mkataba na klabu hiyo kutokana na kutoonekana mazoezini kwa zaidi ya saa 48, hivyo kuvunja kipengele katika mkataba wake.
“Yanga inatangaza rasmi kuwa haitakuwa na kipa Juma Kaseja kwa sababu amevunja mkataba na klabu yetu na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya  huko aendako,” alisema Muro
Kuhusu madai kuwa Kaseja anaidai Yanga, Muro alifafanua: “Kaseja alisaini mkataba na klabu Novemba 8, 2013, siku hiyohiyo akalipwa shilingi milioni 20, makubaliano ilikuwa alipwe shilingi milioni 40 ndani ya kipindi cha mkataba wake wa miaka miwili na hakukuwa na muda maalum uliopangwa.
“Januari 15, 2014 klabu ikamlipa fedha zake zilizosalia shilingi milioni 20, lakini Novemba 11, 2014, akaleta barua ya malalamiko kadhaa kwetu akidai hapati nafasi ya kucheza jambo ambalo siyo kweli na alilalamika kuhusu masuala ya bima.
“Desemba 15, 2014, Klabu ya Yanga ilimjibu barua hiyo na kumfafanulia kile alichohitaji, lakini yote kwa yote hakuna ambacho anatudai wala tunachomdai.”Baada ya hapo gazeti hili lilipata taarifa za ndani juu ya mpango huo wa Yanga kumshitaki Kaseja kwa kukiuka masharti ya mkataba, lakini alipoulizwa Muro alisema hajui chochote kuhusua suala hilo.

0 comments: