Dk Slaa kupanda ‘kizimbani’ leo SOMA HAPA


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, leo anatarajiwa kupanda kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Hai kutoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili kijana aliyejifanya Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Hai, Dennis Mpelembwa alisema jana kuwa Dk Slaa amethibitisha kuitikia wito huo wa Mahakama.
Katika ushahidi uliotolewa mahakamani, Dk Slaa akiwa Mtendaji Mkuu wa Chadema, ndiye anayedaiwa kushughulikia suala la mshtakiwa kutaka kuwatapeli viongozi wa Chadema.
Tayari Jaji Samatta na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wamekwishatoa ushahidi wao katika kesi hiyo inayoendeshwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Katika ushahidi wake, Jaji Samatta alikana kumfahamu mshtakiwa Abeid Adam Abeid (22) na kwamba namba ya simu iliyotumiwa kujitambulisha kwa Dk Slaa na Lema kuwa ni Jaji Samatta siyo yake.
Kwa upande wake, Lema alidai mshtakiwa huyo alimtumia meseji mbalimbali akijitambulisha kwake kuwa ni Jaji Samatta na kwamba angemsaidia katika rufaa yake ya kuvuliwa ubunge ya mwaka 2012.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Takukuru, Susan Kimaro ulidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Aprili na Mei 2012. Mtuhumiwa alikana mashtaka hayo na leo upande wa mashtaka unatarajiwa kufunga ushahidi wao baada ya Dk Slaa na shahidi mwingine ambaye hajatajwa, kutoa ushahidi wao.

0 comments: