ESCROW: KIGOGO AMBAYE NI MENEJA Misamaha ya Kodi TRA MUTABINGWA APATA DHAMANA



MENEJA Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa anayekabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh 1.6 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.

Hakimu Mkazi, Frank Moshi jana alimuachia huru Mutabingwa baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha fedha taslimu Sh 1bilioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Mutabingwa aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kuwasilisha hati tano za nyumba za watu mbalimbali zenye thamani ya Sh 1.332 bilioni, wadhamini watatu ambao kati yao wawili walikuwa wafanyakazi wa TRA na mmoja mjasiliamari.

Kila mdhamini kati ya wadhamini hao, kila mmoja alisaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya Sh340 milioni na mshtakiwa huyo aruhusiwi kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.

Baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu Moshi alimuachia huru mshtakiwa huyo na akaiahirisha kesi hadi Januari 29,2015 ambapo mshtakiwa huyo atasomewa maelezo ya awali (PH).

Awali akisomewa hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo alidaiwa kuwa alitenda makosa ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)(a) cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai akimsomea mashtaka hayo yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda kuwa Januari 27, 2014 katika Benki ya Mkombozi wilaya ya Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba 00110202613801.

Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo akiwa katika Benki ya Mkombozi alijipatia kiasi hicho cha fedha ambacho ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alizipokea kutoka kwa James Burchard Rugemalira ambaye ni Mshauri huru wa Kitaalam, Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni mali ya Rugemalira mahakamani kitu ambacho ni kinyume cha sheria

0 comments: