IKULU YASEMA ITATEKELEZA MAAZIMIO YA BUNGE KWA NGUVU KUBWA....YASUBIRI TAARIFA RASMI ILI RAIS ACHUKUE UAMUZI


SIKU chache baada ya Bunge kuhitimisha mjadala wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kupitisha maazimio nane ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha watendaji na wanasiasa waliohusika, Ikulu imesema itayafanyia kazi maazimio hayo kwa uzito mkubwa.
 
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alipozungumza na MTANZANIA juu ya hatua iliyofikiwa katika kutekeleza maazimio yaliyofikiwa na Bunge.
 
Balozi Sefue alisema hadi sasa ofisi yake ilikuwa haijayapokea maazimio hayo rasmi kutoka bungeni.
 
MTANZANIA: Baada ya Bunge kufikia maazimio yake, ni hatua gani inafuata kwa upande wa Serikali hadi kuja kuyatekeleza?
Balozi Sefue: Ninavyojua ni kwamba Bunge litaleta rasmi mapendekezo hayo serikalini.
 
MTANZANIA: Ni muda gani utatumika kuyafanyika kazi baada kuwasilishwa rasmi serikalini?
Balozi Sefue: Siwezi kusema ni muda gani.
 
MTANZANIA: Kuna taarifa mabadiliko yatafanyika wakati wowote ndani ya juma hili, kuna ukweli wowote?
Balozi Sefue: Nasema hivi, kwanza hatujayapokea, lakini nikiyaona rais atayatafakari na kuyashughulikia, watu wasihisi kwamba ni leo, kesho au lini.
 
Maana ukiyasoma kwa nilivyoyasikia ni kwamba  wametoa ushauri, kwahiyo aliyeshauriwa ndiye atajua afanye nini na kwa wakati gani.
 
MTANZANIA: Kuna wasiwasi kuwa yawezekana huu ushauri usitekelezwe, hilo unalizungumziaje?
Balozi Sefue: Ndiyo nasema wewe soma vizuri lugha iliyotumika, kwa sasa hivi nasoma kwenye magazeti, lakini itakuja rasmi kiserikali, ikiwa rasmi wakati huo rais naye atayasoma na kujua cha kufanya.
 
Ushauri ni ushauri, lakini ushauri wa Bunge lazima uchukuliwe kwa uzito unaostahili, ndiyo ninachoweza kusema, hauwezi kuchukuliwa ‘lightly’ (kiwepesi), lazima utachukuliwa kwa uzito unaostahili, siwezi kukwambia kwamba rais ataamua vipi, ninachokwambia ni kwamba hawezi kuuchukulia ‘lightly’, ataupa uzito unaostahili.
 
DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amelipongeza Bunge kwa hatua iliyofikiwa huku akitilia shaka utekelezaji wa maazimio hayo kutokana na kile alichokiita ‘udhaifu’ wa Serikali katika kutekeleza uamuzi wake.
 
Alisema hofu yake juu ya utekelezaji wa maazimio hayo inatokana na ukweli kwamba mamlaka ya uteuzi imekuwa ikifanya maridhiano na wezi wa mali za umma na kumalizana kienyeji huku wezi wa kuku wakifungwa.
 
“Nimeweka kipimo cha kuangalia mamlaka ya uteuzi itachukua muda gani kutekeleza maazimio haya ya Bunge kwa sababu wajibu wa Bunge ni kusimamia Serikali na si kuhukumu.
 
“Kwa hatua hii, tumetengeneza taswira mbaya kwa kugeuza jinai kwa maridhiano kwa sababu tayari rais alishawahi kusema ana majina ya watu 40 wanaohusika na ujangili wa meno ya tembo, wasafirishaji dawa za kulevya na waliochukua fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
 
“Jambo la kushangaza hadi leo watu hao hajawataja na waliohusika na EPA aliwaomba warudishe fedha walizochukua, yaani watu ambao ni wezi wanapewa muda wa kwenda kujirekebisha, hii ni katiba ya nchi gani?”alihoji Dk. Slaa.
 
Aidha Dk. Slaa alisema taifa halina kumbukumbu na hiyo imethibisha wazi kwamba maazimio ya Bunge huwa hayatekelezwi kutokana na moja ya mapendekezo ya Bunge ya kuitaka Serikali kuutaifisha mtambo wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Solution Limited (IPTL) kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
 
NCCR-Mageuzi
Kwa upande wake Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema kinaunga mkono maazimio hayo ambapo pia kimehoji uhalali wa kumwacha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
 
Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe, alisema kuna mawaziri hawajui yanayotendeka katika wizara zao, lakini wamekuwa wakiwajibishwa na kuwajibika kutokana na makosa ya watendaji wao.
 
“Pinda alikuwa na taarifa zote kuhusu Akaunti ya Escrow, lakini hakuwajibishwa, kwanini ameachwa wakati kuna mawaziri hawajahusika, lakini wamewajibika?
 
“Lakini pia upinzani unatakiwa upewe pongezi nyingi katika hili kwa sababu wameonyesha uwezo wa kujenga hoja na wakasikika bila kutoka nje wala kusussia vikao,” alisema Nyambabe.
 
MAAZIMIO YA BUNGE
 
1) Harbinder Singh Seth (Mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power, PAP) na wengine
Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa) Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi, dhidi ya watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.
 
2 Mitambo ya IPTL
Bunge linaazimia kwamba, Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme wa IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu wa sheria za nchi.
 
3 Mapitio ya Mikataba ya Umeme (Azimio la Kamati teule ya Richmond)
Bunge linaazimia kwamba, Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti la Mwaka 2015/2016, Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
 
4 Kitengo cha Rushwa kubwa
Bunge linaazimia kwamba; Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
 
5 Majaji
Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
 
6 Benki ya Stanbic na Benki nyingine
Bunge linaazimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of Money Laundering Concern).
 
7 Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu na Bodi ya Tanesco
Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
 
8. William Ngeleja, Victor Mwambalaswa na Andrew Chenge

Bunge linaazimia kwamba, kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao kwenye kamati husika za kudumu za Bunge.

Chanzo: Mtanzania

0 comments: